Post by Onyango Oloo on May 2, 2015 18:06:59 GMT 3
UJUMBE WA SDP KWA WAFANYIKAZI
WA SIKU KUU YA WAFANYIKAZI - LEBA DEI:
Mwito wa Karl Marx
WA SIKU KUU YA WAFANYIKAZI - LEBA DEI:
Mwito wa Karl Marx
Enyi wafanyikazi
Wafanyikazi wavujajasho
Mnaomenyeka katika viwanda vya mabeberu
Mnaokamuliwa jasho na mabepari
Huko Nairobi na Mombasa na Kisumu na Eldoret na Thika
Na Nakuru na Nanyuki na Athi River na Kitengela na Naivasha na Machakos
Mnaotumika katika mashamba viwanda vya miwa
Mumias na Miwani na Muhoroni na Nzoia na Soni
Mnaovuja jasho katika mashamba ya chai
Kericho na Limuru na Kisii na Nyeri na Murang'a
Katika mashamba ya kahawa
Kiambu na Murang'a na Kisii na Embu na Meru na Kirinyaga
Wafanyikazi katika mashamba ya mahindi na ngano
Transnzoia na Uasingishu na Nakuru na Bungoma na Narok
Mnaofanya kazi usiku na mchana katika mashamba ya mikonge
Mwatate na Taveta na Voi na Kibwezi na Kilifi
Katika mashamba ya Korosho Pwani
Katika mashamba ya mananasi Thika
Katika mashamba ya maua Naivasha na Adhi River
Katika mashamba ya mifugo Taita na Laikipia na Nakuru
Wafanyikazi katika mahoteli ya watalii
Nairobi na Mombasa na Malindi na Nyeri na Bura na Tsavo
Na Amboseli na Lodwar na Kisumu na Nakuru na Naivasha
Wafanyikazi wa migodi
Magadi na Athi River na Bamburi na Taita na Iteni
Wafanyikazi wa bandarini na maofisini na vyuo vya elimu
Wafanyikazi wa ujenzi wa nyumba na barabara
Wafanyikazi wote wa Kenya
Wafanyikazi wa Afrika Mashariki
Wafanyikazi wa Afrika
Wafanyikazi wa ulimwenguni
Popote pale mlipo duniani
Endeleeni kuuitikia mwito wa Karl Marx:
Enyi wafanyikazi
Wavujajasho wa ulimwenguni kote
Kutokana na juhudi zenu
Kutokana na kutiririka kwa jasho lenu
Kutokana na kumenyeka kwa viungo vyenu
Tunakula
Tunavaa
Tunalala
Tunasafiri
Tunaburudika na kustarehe
Mikono yenu inachora dunia yetu
Kwa bandari na barabara na reli na barste tilatila
Misuli yenu inatupambia sayari yetu
Kwa nyumba na majumba na magorofa mzomzo
Jasho linalomtiririka
Linatupa magari na meli na ndege na vyombo sufufu
Na makompyuta na mitambo na mashini za kila aina
Hakika kazi yenu wafanyikazi
Ndiyo inayotafsiri sayansi na tekinolojia
Katika lugha halisi ya uzalishaji
Kwani nyinyi, enyi wavujajasho popote pale mlipo
Nyinyi ndiyo shina la utamaduni halisi
Ndiyo damu na mifupa ya uhai wa jamii
Ndiyo pumzi na nyenzo za maendeleo ya binadamu
Pasipo nyinyi, enyi wafanyikazi popote pale mnapoishi
Pasipo kazi yenu, jitihada zenu
Kila kitu kitasimama, hata maisha ya ustaarabu
Kwa vile nyie mnaoitwa wafanyikazi, wavujajasho
Nyinyi ndiyo msingi hasa
Wa ungwana na ustaarabu uliyoko duniani
Ndiyo nguvu zinazosababisha mageuzi
Wafanyikazi mu wasanii wa kubadilisha sura ya maumbile
Kwa bidii yenu
Matunda ya ufanisi wa sayansi na tekinolojia yanaliwa
Ndiyo, kazi- nguvukazi
Ndiyo iliyomuumba mtu
Kazi ndiyo iliyomleta binadamu akawa binadamu
Ndiyo iliyomkokota kutoka kwa maumbile
Ikamtenganisha na mnyama
Na kumtia katika mkondo wa historia
Kwa kazi yenu, enyi wafanyikazi tangu kale na sasa
Tunazidisha pengo kati yetu na wanyama
Kwa hivyo, wafanyikazi
Enyi wavujajasho, wazalishaji mali
Tambueni umuhimu wenu!
Tambueni umuhimu wenu wafanyikazi popote pale mlipo!
Bila nyinyi hakuna historia
Pasina uzalishaji na wazalishaji maisha yatasimama
Lakini
Enyi wafanyikazi
Enyi wafakazi mnaokufa kwa kazi
Wafanyikazi wa nchi yangu
Wafanyikazi wa Afrika Mashariki
Wafanyikazi wa Afrika bara langu
Wafanyikazi wa ulimwenguni kote
Ulimwengu uliyotekwa nyara na mfumo wa kinyama wa ubeberu
Katika mataifa yaliyoko chini ya ukoloni-mamboleo
Penye jamii ya mfumo wa mwenyenguvu mpishe mnyonge msonge
Wafanyikazi mnaishi maisha magumu mno, maisha ya kinyama
Mmegeuzwa watumwa katika nchi zenu wenyewe
Maisha yenu enyi mfanyaokazi
Enyi mmenyekao
Enyi wafanyikazi wa Kenya taifa langu
Enyi wazalishaji chini ya ubepari na ubeberu
Ni maisha ya tabu dhiki na kusaga meno
Maisha ya umaskini ufukara na ukosefu
Maisha ya njaa na kiu cha kila mazuri
Maisha machungu ya upweke na ukiwa
Maisha ya ushenzi ushirikina ulevi na ujinga
Maisha ya kugandamizwa na kunyanyaswa mbele na nyuma
Maisha ya hofu wasiwasi kiherehere na dukuduku
Maisha ya kutumiwa kutukanwa kudhalilishwa na kuonewa
Maisha ya kunyonywa na kutajirisha waajiri wenu
Maisha ya kuzalishia wachache katika jamii
Maisha chini ya imla na kuvunjwa kwa haki za binadamu
Maisha ya mashindano na mapambano kila kuchako
Enyi wafanyikazi wa Kenya, nchi yangu mzazi
Enyi wafanyikazi wa Afrika, bara linalochemka kwa ghamu na ghadhabu
Enyi wafanyikazi chini ya himaya ya ubeberu na ubepari
Mnaishi kwa shida, shida tupu
Shida ya inflesheni na ujira wa kitumwa
Shida ya kupunjwa na kulanguliwa juu na chini
Shida ya kutafuta karo za shule
Shida ya maradhi na kukosa dawa na matibabu
Shida ya ajali barabarani na viwandani
Shida ya ukosefu wa nyumba na kunyonywa na wenye nyumba
Shida ya uhalifu na wahalifu na maisha ya kimathare mijini
Shida ya machugachuga na mahangaiko ya ukosefu wa kazi
Shida ya kukamatwa kuteswa kufungwa na kuuawa na wahalifu na polisi
Shida ya ukabila upendeleo na ubaguzi wa rangi
Shida ya ubaguzi wa kijinsia na kunyanyaswa kwa wanawake
Shida ya kutawalwa na wakora wasaliti walafi wajinga
Shida ya hofu ya nyakati za uzeeni
Maisha ya shida ghasia mizozo na gandamizo
Hamna raha ndugu wafanyikazi hamna katu hamnani
Matunda ya jasho lenu yanaliwa na mabepari na jamaa zao
Utamaduni halisi mnaouzalisha ni kwa ajili ya tabaka la wanyonyaji
Oh wafanyikazi wa nchi yangu
Mnaonyonywa katika viwanda vya mabeberu nchini
Mnaotumishwa katika mahoteli ya mabepari wa kimataifa
Mnaochapishwa kazi kwa mashamba ya wakoloni-mamboleo
Mnaohangaishwa katika makampuni na biashara za wageni
Umaskini wenu ni utajiri wa Ulaya, Marekani na Japan
Jasho lenu linafaidi mataifa yanayotunyonya
Juhudi zenu hazitumiki kuboresha maisha katika taifa lenu
Mazao ya akili na misuli yenu yanang'wafuliwa na wanyonyaji wa nje
Dola la Kenya linashikilia na kulinda mirija ya kuwakamua
Serikali ya mahomugadi wa jana na leo inawasaliti kwa maadui zenu
Nalo tabaka la matajiri wa kienyeji ni waitifaki wa ubeberu
Mnauzwa na ndugu zenu wenyewe kwa pesa nane
Oh wafanyikazi wa nchi yangu ya kuzaliwa
Wafanyikazi wa Afrika Mashariki na Afrika
Ubeberu unamnyonya kama wafanyikazi na watu weusi
Unatumia ukabila na ubaguzi wa rangi kuzidisha kunyonywa kwenu
Enyi wanawake wafanyikazi wa nchi yetu
Mnanyonywa kama wafanyikazi kama watu weusi na kama wanawake
Mnaelewa hali yenu wafanyikazi mnajua ukatili mtendewao
Nyanyaso mnazonyanyaswa mnazielewa zaidi
Maonevu mnayoonewa mnayafahamu sana
Vilio mnavyolia mnaweza kuvieleza kwa marefu na mapana
Wambea wenu mnaishi nao mnajua ukatili wao juu chini
Itikadi na mbinu za kuwarubini lazima mzibaini bayana
Kwani daima mko katika harakati za kitabaka
Maadamu mazao yenu yanazidisha utumwa na mateso yenu
Na chini ya ukoloni-mamboleo
Chini ya dola la vibaraka wa mabeberu
Chini ya udikteta na ufashisti wa wasaliti
Hamna hata haki ya kuuza jasho lenu, sembuse uhuru!
Mwanyonywa vururumtende kwa msaada wa dola la wauzaji wa nchi
Polisi wanatumiwa kuvunja migomo na maandamano yenu
Sheria zimetungwa kuhalalisha kunyonywa na kunyanyaswa kwenu
Jela zinatumiwa kuwafunga mashujaa na waitifaki wenu
Propaganda zinasambazwa za kuwadanganya na kuwagawanya
Mnaleweshwa elimu ya ubepari na ushirikina kuparaganya mapambano yenu
Vyama bandia vya wafanyikazi vilivyoundwa na serikali
Vinamsaliti vinamuuza hadharani usiku na mchana
Enyi wafanyikazi wa Kenya
Msiosita kupambana
Hamna chama chenu cha wavujajasho hamna mnasema kila siku
Udikteta, utawala wa mbwa wa wanyonyaji wa nchi yetu
Unawapora haki yenu ya kuunda vyama huru vya wafanyikazi
Enyi wafanyikazi!
Wafanyikazi wa Kenya!
Wafanyikazi wa Afrika!
Wafanyikazi wa ulimwenguni!
Mna uwezo mkuu wa kujikomboa
Nguvu zenu zatosha kuvunja silisili zinazomfunga
Nyie ndie mnaoshikilia bomubomu
Za kuulipua mfumo wa kinyama wa kibepari
Ndiyo silaha kuu
Za kutukomboa kutoka kwa nyanyaso za ubeberu
Enyi wafanyikazi wa Kenya
Mliyoongoza mapambano ya uhuru
Mliyoshikilia tochi ya ukombozi katika vita vya Mau Mau
Hata leo jukumu ni lenu wafanyikazi
Hamna budi kuendelea kuwa katika mstari wa mbele
Katika vita dhidi ya udikteta na ukolonimamboleo
Wafanyikazi wa Afrika na dunia inayonyonywa na ubeberu
Wavujajasho na ndugu zenu wakulima-makabwela
Mnaonyonywa kuliko wafanyikazi katika nchi za kibepari
Mnaonyanyaswa kama wafanyikazi na kama taifa
Hakika ukombozi wenu ndiyo utakaokuwa msingi
Wa ukombozi wa wafanyikazi wa Ulaya na Marekani na Japan
Ukombozi kamili wa wote wanaonyanyaswa duniani
Enyi wafanyikazi
Nyinyi ndio mizizi ya kuhakikishia dunia
Kuchipuka na kukua kwa huru haki amani na furaha kamili
Wafanyikazi wa Kenya
Nyie ndio shina
Ya harakati za kidemokrasi
Pambaneni! Pambaneni! Pambaneni!
Popote mlipo nchini
Pambaneni! Pambaneni! Pambaneni!
Msirudi nyuma wala msikate tamaa hata siku moja
Pambaneni! Pambaneni! Pambaneni!
Usiku na mchana pambaneni!
Kupambana ni haki yenu pambaneni wafanyikazi wa Kenya!
Pambaneni dhidi ya waajiri na matajiri!
Pambanieni ujira bora na bora zaidi!
Pambanieni hali bora ya kuuza nguvukazi yenu!
Pambanieni haki ya kuwa na vyama huru vya wafanyikazi!
Pambanieni haki ya kuchagua viongozi wenu wenyewe!
Pambanieni haki ya kukutana kugoma na kuandamana!
Pambaneni dhidi ya wasaliti wanaomuuza kwa wanyonyaji!
Pambaneni dhidi ya vyama bandia mnavyoundiwa na dola!
Pambaneni dhidi ya mfumo wa imla!
Pambaneni dhidi ya kasumba ya kikoloni!
Pambaneni dhidi ya itikadi za kibwanyenye!
Pambaneni dhidi ya utamaduni wa hofu na kimya!
Pambaneni dhidi ya ukabila na ubaguzi wa rangi!
Pambaneni dhidi ya unyanyaswaji wa wanawake!
Pambaneni kwa matumaini ya ushindi wa ukombozi kamili
Hakika usoshalisti ndiyo mwokozi wenu
Ukomunisti ndiyo ukombozi kamili wa dunia upambanieni!
Itikadi ya Umarx-Ulenin daima iwe tochi na ngao yenu
Mapinduzi tu
Mapinduzi ya kisoshalisti
Ndiyo yatakayotuhakikishia uhuru wengi tunaonyonywa
Demokrasi ya kibepari isiwe mwisho wa mapambano yenu
Demokrasi iwe ngazi ya kuuvunjilia mbali mfumo wa kinyama wa ubepari
Demokrasi ya tabaka la wengi wanaonyanyaswa, dola linalodhibitiwa na wafanyikazi
Dola la kung’oa mizizi yote ya mfumo wa ubepari na ukoloni-mamboleo
Dola la kujenga na kulinda mfumo wa usoshalisti
Ndiyo shabaha ya harakati za kidemokrasi ya wafanyikazi
Pambaneni! pambaneni! pambaneni!
Pambaneni huku mkikumbuka umuhimu wenu kama wafanyikazi!
Pambaneni bila kusahau ndugu zenu wa kitabaka wakulima-makabwela!
Umoja wenu
Mshikamano madhubuti wa wavujajasho
Muungano wa wanaonyonywa na kugandamizwa
Usiojua kabila wala rangi
Unaokataa kubaguliwa kwa wanawake
Wenye kushikanishwa na gundi ya itikadi ya ukomunisti
Ndiyo silaha na hakika yenu ya ushindi!
Enyi wafanyikazi wachimbaji wa kaburi la ubepari
Mtakaozika mfumo wa udhalimu wa mtu kwa mtu
Unganeni! Unganeni! Unganeni kwa mapambano!
Popote mlipo unganeni wanaonyanyaswa wote!
Unganeni mpambane pasina kurudi nyuma
Hamna chochote cha kupoteza
Isipokuwa dhiki na nyanyaso za ubepari na ukoloni-mamboleo!
Hakika mapinduzi yenu wafanyikazi
Yatakuwa msingi wa kujenga mbingu hapa hapa duniani!
Yadumu mapambano ya wafanyikazi!
Zidumu harakati za uhuru wa wananchi wengi wa Kenya!
Udumu ukomunisti!
Adumu Makhan Singh, mkomunisti wa kwanza Kenya
Wadumu kina Chege Kibacia na Pio Gama Pinto na Isaak Gathanju
Na kina Harry Thuku na Bildad Kaggia na Mary Muthoni Nyanjiru wadumu
Wadumu mashujaa wa wafanyikazi wa Kenya
Yadumu majina ya kina Marx, Engels, Lenin na Stalin!
Wadumu kina Mao Tse Tung na Kim Il Sung na Fidel Castro na Che Guevara
Na Chris Hani na Julius Nyerere na Samora Machel na Amilcar Cabral na Agostino Neto
Na Kim Jong Il na Walter Rodney na Maurice Bishop wadumu na Joe Slovo
Zidumu fikra za kina Kwameh Nkuruma na Abdulrahman Mohamed Babu na Mamdani
Na fasihi za kina Shiraz Duran na Ngugi wa Thiong’o na Sembene Ousman
Na Shafi Adamu Shafi na Alex Laguma na Shaaban Robert na Chinua Achebe zidumu
Na zile za kina Felix Iyayi na Ahmed Said Mohamed na Ayi Kwei Armah zidumu pia
Zidumu fikra za kimapinduzi na mapinduzi Afrika
Na muungano wa kimapinduzi wa Afrika udumu
Wadumu wakomunisti popote walipo nchini na ulimwenguni!
Udumu umoja wa wafanyikazi wa kupambania ukombozi wa jamii!
Na iwe ni aluta Kontinuaaahhh hadi ukombozi kamili
Kenya
Na duniani!
Social Democratic Party of Kenya (SDP)
Mei 1 2015