Post by Onyango Oloo on Jul 7, 2014 16:32:04 GMT 3
The poet
Abdilatif Abdalla has just emailed me the following, to give more context to the above dramatic presentation of his famous poem:
RISALA KWA WASHIRIKI KATIKA TAMASHA LA KITAMADUNI LA LAMU
Wazee wangu, Ndugu zangu, Mabibi na Mabwana,
Assalaam alaykum warahmatuLlahi wabarakaatuh. Ni furaha kuu kwangu kupata nafasi hii ya kuwaamkua na kusema nanyi maneno machache. Laiti nami ningekuwa miongoni mwenu hapo Lamu, na kushirikiana nanyi katika Tamasha hili. Lakini, chembelecho waliosema, "Safari ni khatua." Sikupata khatua ya kuwa hapo Lamu.
Mabibi na mabwana, usiku wa leo mumejumuika hapo Mkunguni ili kulisikiza na kulitizama shairi langu, Mnazi: Vuta N'kuvute, likiigizwa. Kwamba tukio hilo latokea hapo Lamu, kwangu mimi ni fakhari na hishima kubwa. Kwani Lamu, na Faza, ni visiwa ambavyo vina hisa kubwa na tangizo kubwa katika maisha yangu.
Kiasi cha miaka khamsini na sabaa iliyopita, nikiwa ni mtoto wa kiasi cha miaka sita, nilipitia hapo Lamu kwa jahazi kwendea Faza, kutoka kwetu Mombasa, pamoja na walezi wangu - yaani babu yangu, Sheikh Ahmad Basheikh, na mkewe, Bi Sharifa Haji Fadhil. Babu yangu huyu alikuwa ni miongoni mwa walimu wa mwanzo waliopelekwa Faza kuanzisha skuli ya msingi hapo. Basi hapo Faza ndipo nilipoanza kusomeshwa alif bee na a b c d.
Baada ya miaka michache, tukaguria Lamu - ambapo babu yangu alisomesha skuli ya hapo kwa kiasi cha miaka mitatu hivi; nami nikawa naendelea kusoma skuli. Kwa hivyo, basi, visiwa vya Faza na Lamu vina hisa yake kubwa kwangu; nami sina malipo yawezayo kutosheleza kuvilipa. Isipokuwa kuzidi kuviombea Mwenyezi Mngu avipe ufanisi na kila lililo na kheri navyo, pamoja na wakazi wake; Ammiyn.
Kama mtakavyolisikia, Mnazi: Vuta N'kuvute ni shairi likhusianalo na mvutano baina ya pande mbili za jamii:
Upande wa kwanza - ambao katika shairi hili wawakilishwa na Badi - ni upande wa wale walafi wasiokinai. Watu hawa dini yao ni kuwadhulumu na kutowajali wenzao; na Mngu wao ni mali.
Na upande wa pili - ambao wawakilishwa na Alii - ni upande wa wale walio wanyonge katika jamii, walio hohe hahe, wasiokuwa na mbele wala nyuma, kwa sababu ya hao walafi kukibwakura kila wakionacho, na ambacho ni mali ya jamii nzima!
Shairi hili ni miongoni mwa mashairi niliyoyatunga nilipokuwa katika Gereza la Kamiti (karibu na Nairobi), na Gereza la Shimo la Tewa, (Mombasa), baina ya mwaka 1969 na mwaka 1972; na baadaye mashairi haya yakachapishwa katika kitabu nilichokiita Sauti ya Dhiki.
Sababu za kufungwa kwangu zilitokana na harakati za kuipinga serikali ya wakati huo kwa sababu ya mwendo wake mbaya na siasa zake mbaya. Serikali hiyo ilikuwa ikiongozwa na Rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, pamoja na chama cha KANU.
Katika mwezi wa Disemba mwaka 1968, nikayaandika, na kuyachapisha, na yakasambazwa kwa siri, makala niliyoyaita, Kenya: Twendapi? Haya yalikuwa ni makala ya sabaa miongoni mwa mfululizo wa makala niliyokuwa nikiyaandika kila mwezi kuelezea siasa za KPU, na pia kuitoa makosa serikali kwa iliyokuwa ikiyafanya. Haya ndiyo makala yaliyosababishwa mimi kushikwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani.
Kama tujuavyo, Kenya ilipata uhuru wake katika mwaka 1963. Uhuru ambao ulipiganiwa kwa Wakenya kutoa jasho lao, kutoa kila walichonacho, na pia kutoa roho zao ili kupigania haki ya kujitawala na kupinga dhuluma za kila namna walizokuwa wakifanyiwa na utawala wa kikoloni wa Mwingereza. Matarajio yalikuwa ni kwamba upatikanapo uhuru, maonevu hayo na dhuluma hizo nazo zitakoma.
Lakini miaka miwili tu baada ya uhuru, baadhi kubwa ya waliokuwa wameshika nyadhifa za juu katika serikali hiyo ya Kenya huru, wakaanza kwenda kinyume kabisa na malengo ya asili ya kuleta haki na usawa katika jamii yetu. Miongoni mwa vitendo vichafu na vya dhuluma kubwa walivyokuwa navyo ni kunyakua na kulimbikiza mali na kujitajirisha wao binafsi na jamaa zao waliokuwa karibu nao, bila ya kuwajali wananchi wenzao, ambao wengi wao walikuwa katika hali ya umasikini.
Katika serikali hiyo, lakini, walikuwamo viongozi wachache ambao hawakukubaliana na vitendo vya serikali hiyo. Miongoni mwao alikuwa ni Makamu wa Rais wa kwanza, Jaramogi Oginga Odinga. Baada ya yeye na wenzake kushindwa kuzibadilisha nyendo za serikali hiyo wakati wamo humo serikalini, katika mwaka 1966 walijiuzulu na kukaundwa chama cha upinzani kilichoitwa Kenya People's Union (yaani KPU), kilichoongozwa na Oginga Odinga. Wakati huo umri wangu ulikuwa ni miaka ishirini; nami nikawa mwanachama na mwanaharakati wa KPU. Miongoni mwa malengo makuu ya chama hicho yalikuwa ni kwamba uchumi wa nchi usiwe mikononi mwa watu wachache tu bali uwafaidi Wakenya wote. Baada ya miaka mitatu tu (katika mwaka 1969) serikali ilikipiga marufuku KPU, na viongozi wake wakashikwa na kuwekwa kizuizini.
Mwezi ujao, tutatimiza miaka 46 tangu Kenya ilipopata uhuru wake. Jambo la kusikitisha sana ni kwamba kwa baadhi kubwa sana ya Wakenya hali iliyokuwako nyakati hizo ndiyo iliyoko mpaka sasa. Bali naweza kusema, tena bila ya kugigisa, kwamba hali ya Wakenya hao hivi sasa ni mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa nyakati hizo. Hakuna atakayeweza kuibadilisha hali hiyo isipokuwa Wakenya wenyewe.
Kwa ufupi, basi, katika shairi hili, Mnazi: Vuta N'kuvute, Badi ni Mzee Jomo Kenyatta na kundi lake la wasiokinai, na Alii ni Jaramogi Oginga Odinga na kundi lake la Wakenya ambao wataka mabadiliko katika jamii yetu ili kila Mkenya afaid**e kwa kuishi maisha ya kibinaadamu na maisha ya hishima.
Matumaini yangu, khaswa kwa vijana, ni kwamba tutaisoma historia yetu tuielewe vizuri, na pia kwamba tutajifunza kutokana na historia hiyo ili makosa yaliyotendeka hapo zamani yasiwe yakirudiwarudiwa, ili kupatikane mabadiliko ya kweli katika nchi yetu - mabadiliko ambayo yatamfaidi kila Mkenya bila ya kujali kabila lake, au rangi yake, au dini yake. Sote tumo katika dau moja, na kwa hivyo dua yetu lazima iwe ni moja!
Nawashukuru sana kwa kuja kuwasikiza wasanii wetu wakiliigiza shairi hili.
Ni mimi mwenenu na mwenzenu,
Abdilatif Abdalla Leipzig Ujerumani Tarekhe 21 Novemba, 2009
Last Edit: Jul 7, 2014 16:37:13 GMT 3 by Onyango Oloo